Welcome

    Featured Posts

    BURUDANIKA BLOG - KWA MICHEZO NA BURUDANI ZOTE

    .

Loading...

SIMBA HOI KWA KAGERA SUGAR, CHEZEA MIWA WEWE MNYAMA!!!

TIMU ya Kagera Sugar imevunja mwiko wa Simba kutofungwa katika msimu huu kwa kuichapa bao 1-0 na kufanya kocha wa wanamsimbazi Patrick Phiri kurudi katika hali ya presha ya kuweza kusitishiwa kibarua chake.
Pia baada ya kuisha mchezo mlinda mlango wa Simba, Ivo Mapunda alitolewa uwanjani kwa kusindikizwa na polisi kutokana na mashabiki wenye hasira kumtolea vitisho kwa kumlaumu kufanya uzembe uliosababisha timu yao kufungwa.
Bao pekee la Kagera Sugar katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kuifanya timu hiyo kumaliza mwaka kwa kufungwa mchezo mmoja liliwekwa wavuni na Atupele Green dakika ya 21.
Mfungaji huyo aliunganisha kwa shuti mpira wa kurushwa na Benjamin Asukile huku mlinzi wa Simba Hassan, isihaka akiusindikiza mpira wavuni.
Kwa matokeo hayo Simba, imeshinda mechi moja, kufungwa moja, kutoka sare sita na imebaki na pointi tisa na kubakia nafasi ya saba huku Kagera Sugar ikifikisha pointi 13 na kuingia kwenye timu nne za juu.
Kwa ujumla simba imepoteza pointi 15 tangu msimu kuanza katika mechi nane, ilipoteza pointi 12 kwa kutoka sare mechi sita kabla ya kupoteza pointi tatu jana.
Simba ilipoteza nafasi mbili za kufunga dakika ya 4 na 23 kupitia kwa mchezaji wake mpya, Simon Sserunkuma mashuti aliyopiga yalidakwa na mlinda mlango wa Kagera, Agaton Anthony.
Mwamuzi wa kati Andrew Shamba kutoka Pwani ametoa kadi ya njano kwa George Kavila dakika ya 13 baada ya kumfanyia madhambi Ramadhani Singano, dakika ya 14 alipatia kadi hiyo pia Awadhi Juma baada ya kumfanyia madhambi Erock Kyaruzi.
Dakika ya 17 mshambuliaji mpya wa Simba, Dan Sserunkuma nusura angeipatia bao timu yake, shuti alilopiga liliokolewa na mlinzi wa Kagera, Salum Kanoni.
Mlinzi wa Simba kutoka Mtibwa, Kessy Ramadhan alimpasia pasi nzuri
Dan Sserunkuma lakini alishikwa na kigugumizi na mpira kudakwa na mlinda mlango wa Kagera, Anthony ambaye pia alidaka shuti la Okwi dakika ya 45.
Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Kagera ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Dakika ya 50, Phiri alifanya mabadiliko katika kikosi cha Simba kwa kumtoa Awadhi Juma na kumwingiza Shaban Kisiga, dakika ya 70 alimpumzisha Dan Sserunkuma nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla.
Kagera inanolewa na Jakson Mayanja ilimpumzisha Benjamin Asukile baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa Victor Hussein.
Ndemla nusura aifungie Simba bao, dakika ya 77 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Kessy, alipiga shuti na mpira kupaa juu..
Mayanja alifanya mabadiliko mengine kwa kumpumzisha Babu Seif dakika ya 88 baada ya kupoteza fahamu na mpira kusimama dakika 3 , nafasi yake kuchukuliwa na Simon Lucas kabla ya kumtoa Daud Jumanne nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mpola.
Hadi mwisho wa mchezo Kagera ilitoka uwanjani ikiwa na ushindi wa bao 1-0.
Katika mchezo ujao Januari 4 mwakani Simba itacheza ugenini dhidi ya Mgambo wakati Ruvu Shooting itaivaa Kagera Sugar.
Simba: Ivo Mapunda, Kessy Ramadhani, Mohammed Hussein, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Ramadhan Singano, Awadh Juma, Dan Sserunkuma, Simon Sserunkuma na Emmanuel Okwi.
Kagera: Agaton Anthony, Salum Kanoni, Abubakar Mtiro, Eric Kyaruzi, George Kavila, Malegesi Mwangwa, Paul Ngwai, Babu Seif, Atupele Green, Daud Jumanne na Benjamin Asukile.
© Copyright BURUDANIKA BLOG
Back To Top