Welcome

    Featured Posts

    BURUDANIKA BLOG - KWA MICHEZO NA BURUDANI ZOTE

    .

Loading...

WEMA SEPETU ULIFIKIRI MARA NGAPI KABLA YA KUTENDA?!

Kama umeumbwa na moyo wa kibanadamu na ukapata nafasi ya kuona kile alichokiandika msanii maarufu, Wema Sepetu kuhusu suala lake la kutoweza kupata ujauzito basi ni wazi kwamba ulihuzunika sana. 

Hata mimi pia nilihuzinika, lakini nilihisi vibaya zaidi nilipokumbana na maneno yasiyo ya kiungwana yaliyoongelewa kwenye mitandao kumhusu Wema.
Hivi karibuni mwanadada huyo aliyewahi kuwa Miss Tanzania, aliandika katika ukurasa wake wa instagram kuwa hana uwezo wa kupata mtoto. 

Ingawa Wema ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Diamond Platinum hakuweka wazi ni tatizo lipi linalomsibu lakini ukisoma ujumbe huo utagundua kuwa mwanadada huyo huenda amepata taarifa za kitabibu kuwa hawezi kupata mtoto tena katika kipindi cha maisha yake. 

Kutokana na waraka huo, wapo waliomuonea huruma na kumpa pole kutokana na tatizo hilo, lakini pia wapo waliomkejeli na kumwambia kwamba hayo ni matokeo ya matendo yake ingawa sina uhakika kama watu hao wana uthibitisho wa waliyokuwa wakiyasema, ila kwasababu mitandao ya kijamii inatoa uhuru wa kuzungumza chochote unachojisikia, hata kama ni kibaya watu wanaandika kile kinachokuja katika vichwa vyao. 

Lakini nikigeukia kwa Wema, napata maswali mengi sana. Najiuliza alitafakari mara ngapi kabla ya kutenda haya? Aliwaza nini hadi kuandika ujumbe wa namna ile? Je alifikiria athari zake?
Sote tunajua mitandao ya kijamii hivi sasa inavyotumika vibaya. Je, Wema alizingatia hilo? 

Wapo mabingwa wanaosifika kwa tabia za kuwachafua wenzao kwa kutumia mitandao ya jamii. Baadhi ya watu sasa wanashinda kutwa kucha mitandaoni kwa lengo la kuharibu heshima za wengine. Je, hili nalo Wema alikuwa akilijua kabla ya kufanya uamuzi wake? 

Bila shaka lengo lake lilikuwa ni kuwafahamisha wale wote wanaomsema vibaya kwamba hana mtoto kwa sababu anaendekeza ujana, lakini binafsi nahisi amefeli na laiti kama ningekuwa mtu wake wa karibu ningemshauri asiandike kwa mtindo ule alioutumia. 

Naamini sasa ujumbe ule umemsababishia maumivu zaidi ya yale aliyokuwa nayo kabla ya kuandika kwani wengi walitoa maoni ya kumkashifu. 

Wema alitakiwa kufahamu kwamba shabiki si ndugu yake, ni mteja wa bidhaa anayoiuza tu, iwe ni filamu au vingine vyote anavyofanya. Kwa uhalisia sidhani kama muuza genge mwenye tatizo la kufanana na hilo atakuwa akimueleza kila mteja wake anayekuja gengeni kwake kununua nyanya na vitunguu. 

Pia ni lazima aelewe kuwa si yeye pekee mwenye tatizo hilo. Kuna familia nyingi huku mtaani zinahangaika kupata mtoto mchana na usiku. Lakini waathirika wa tatizo hilo hawathubutu kusimama hadharani na kutangaza tatizo lao ingawa jamii inayowazunguka imekuwa ikiwajadili kila kukicha.

Si kwamba ni aibu au fedheha kwa upande wao, bali kwa tamaduni zetu hilo si jambo la kumwambia kila mtu. Hayo ni masuala ya kifamilia na anayepaswa kufahamu ni mke ama mume na wakati mwingine hata wazazi huwa hawashirikishiwi. 

Ningempa ‘Big Up’ kama ujumbe ule angeuandika kwa mtindo wa kutoa elimu kwa mabinti wengine na hiyo huja tu kama amethibitishiwa na daktari chanzo cha tatizo ni nini.
Mfano mzuri ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2001, Happiness Millen Magese. Yeye aliileza jamii kwamba hana uwezo wa kupata mtoto kwa njia za kawaida kwa mtindo tofauti na Wema. 

Magesa Alieleza kwamba chanzo cha tatizo lake ni kudharau maumivu aliyokuwa akiyapata wakati wa hedhi alipokuwa binti mdogo na mwisho akisisitiza wadada wote wasidharau maradhi yanayoonekana kuwa ni madogo kama yeye alivyofanya na pia wanawake wajijengee utaratibu wa kucheki afya zao mara kwa mara hasa.

Mrembo huo aliweza kufikisha ujumbe kwa wasichana wengi kwani yeyote aliyesikia au kusoma, jambo lile lilimpa funzo kubwa la kutodharau mambo. 

Ninachokiona kwa Wema ni tofauti kwani inaonyesha wazi aliandika ujumbe ule akiwa na hasira na siku zote maishani watu wanaofanya uamuzi wanapokuwa wamekasirika, hufanya uamuzi ambao unawaathiri zaidi.

Jiulize ni maumivu kiasi gani aliyoyapa baada ya kuona watu wakitoa ‘comment’ za kumkashifu? Ni wazi kabisa aliendelea kuumia baada ya kusoma mjadala ule. 

Namshauri Wema afike hospitalini ili kuwaona wataalamu wa masuala ya uzazi ambao wataweza kumfanyia vipimo mbalimbali na kugundua tatizo lake hatimaye kumpatia matibabu.
Cha msingi aongeze maombi, kwani kwa kumtegemea Mungu hakuna linaloshindikana. 

Naamaini msanii huyo bado ni binti mwenye uwezo wa kubeba mimba na kuzaa. Ikiwa Sarah alipata mtoto akiwa na umri wa miaka 90, kwanini yeye mwenye miaka isiyozidi 30 avunjike moyo?
© Copyright BURUDANIKA BLOG
Back To Top