
MWANAMUZIKI wa kizazi kipya kutoka mkoani Morogoro Abelnego Damian ‘Belle 9′ amesema kukosa kwake tuzo hakumnyimi usingizi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, mwanamuziki huyo alisema mwanzoni alikuwa anaumizwa na kukosa raha kutokana na nyimbo zake zote alizotoa kuwa nzuri.
Alisema bado anajiuliza ni vigezo gani vinavyotumika ili kumwezesha msanii kupata tuzo.
“Siku za nyuma ndio nilikuwa nakosa raha kutokana na kukosa tuzo lakini kwa sasa naona kawaida”, alisema Belle 9
Vilevile alisema ni muhimu kuendelea kukomaa kufanya kazi kali na nzuri na huenda pengine muda wake wa kupata tuzo bado haujafika.
Msanii huyo anatamba na nyimbo zake kadhaa kama vile Sumu ya Penzi ambao ulifanikiwa kumtambulisha vyema katika ulimwengu wa muziki.