WAKATI Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga, Hans van der Pluijm, akitamba vijana wake watapambana kupata ushindi dhidi ya Etoile du Sahel wa kuwania Kombe la Shirikisho, utakaofanyika kesho Uwanja wa Taifa, klabu hiyo imetangaza viingilio ambapo cha chini ni sh. 5000.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya Klabu ya Yanga, Dar es Salaam jana, Pluijm alisema kikubwa ni kujiamini na kutambua kama wapo mbele ya mashabiki wao wengi, hivyo matokeo mazuri ndiyo njia nzuri kwao.
Alisema wachezaji wake watajiamini na kuhakikisha wanapata ushindi utakaofanya wawe wepesi katika mchezo wa ugenini.
Pluijm alisema zimebaki siku mbili kabla ya kuvaana na wapinzani wao ambao ni moja ya timu nzuri zinazoshiriki michuano ya kimataifa, hivyo nao hawabweteki wala kudharau.
Alisema ana amini kila mchezaji wake yupo vizuri kimchezo, huku akiomba wapenzi wajitokeze kuwapa nguvu zaidi ya kuhakikisha wanapata ushindi mzuri wa mabao mengi.
“Nina amini kila mchezaji amejengeka kimazoezi, hata kinguvu, lakini sapoti ni kitu muhimu, nina amini tunacheza nyumbani matokeo mazuri ndiyo kitu kizuri, nasi tumejipanga kupata ushindi mzuri katika mchezo huo,”alisema Pluijm.
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha Habari cha timu hiyo, Jerry Muro, alisema katika mchezo huo kiingilio cha juu ni sh. 40,000, wakati VIP B itakuwa sh. 30,000, VIP C itakuwa sh. 20,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 10,000 na sh. 5000 viti vya bluu.
Muro alisema tiketi za mechi hiyo zitaanza kuuzwa leo saa 4, asubuhi katika vituo maalumu ambayo huuzwa tiketi za mechi mbalimbali.
Pia Muro alizugumzia wachezaji wao waliokuwa majeruhi, ambapo sasa wanaendelea vizuri.
Alisema mchezaji wao Salum Telela, ambaye aliumia kwenye mchezo wao dhidi ya Mbeya City, anaendelea vizuri.
Muro alisema licha ya kupata nafuu kwa mchezaji huyo hata wachezaji wengine waliokuwa majeruhi nao wapo, vizuri na wanafanya mazoezi na wenzao.
Wachezaji hao ni Mbrazil Andrey Coutinho na Jerryson Tegete, ambao wapo kambini na wenzao na wanaendelea na mazoezi ya pamoja.