Welcome

    Featured Posts

    BURUDANIKA BLOG - KWA MICHEZO NA BURUDANI ZOTE

    .

Loading...

HATARI SANA: LIGI KUU BARA LEO HAPONI MTU!

Kikosi cha Stand.
NA KHADIJA MNGWAI
LIGI Kuu Bara inafikia tamati leo Jumamosi kwa timu zote 14 kucheza mechi zake za mwisho. Hata hivyo, michezo mingi ya leo, itakuwa ya kukamilisha ratiba kwa upande wa kusaka ubingwa na uwakilishi wa mechi za kimataifa.
Mashabiki wa timu ya Yanga SC.
Tayari Yanga ni bingwa kwani ina pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ile, wakati Azam FC ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 48 ambazo hakuna timu inayoweza kuzifikia. Yanga itaiwakilisha Bara katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao huku Azam ikicheza Kombe la Shirikisho.

Simba imejihakikishia nafasi ya tatu na haitashiriki michuano ya kimataifa, lakini vita ipo kuanzia nafasi ya tisa zilipo timu za Ruvu Shooting, Prisons, Ndanda FC, Mgambo JKT, Stand United na Polisi Moro.

Hizo zote zinawania nafasi ya kubaki ligi kuu kwani zikiteleza kidogo tu mambo yanaweza kuwa mengine na inaweza kuwa historia kwani timu iliyo katika nafasi ya pili kutoka chini yaani Stand United inaweza kubaki katika ligi na ile iliyo nafasi ya tisa yaani Ruvu Shooting inaweza kushuka. 

ZILIZO KATIKA HATARI
Ruvu Shooting inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 29 huku ikiwa imefunga mabao 16 na kuruhusu mabao 28 nyavuni kwake.

Kuanzia nafasi ya 10 hadi ya 13 zipo timu nne ambazo ni Prisons, Ndanda, Mgambo na Stand ambazo zote zina pointi 28 ila zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mkiani kwenye nafasi ya 14 ipo Polisi Moro yenye pointi 25 na yenyewe bado inategemea miujiza ya kushinda mechi ya mwisho dhidi ya Mbeya City huku ikiombea wapinzani wao wote kwenye vita ya kubaki ligi kuu wafungwe. 

MECHI ZA KUFA NA KUPONA
Katika mechi za leo, ni mbili ambazo zitakuwa za kukamilisha ratiba tu ambazo ni ile itakayoikutanisha JKT Ruvu na Simba kwenye Uwanja wa Taifa pamoja na Mtibwa Sugar na Coastal Union Uwanja wa Manungu, Turiani.

Kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, wenyeji Stand watacheza na Ruvu Shooting. Ruvu ina pointi 29 na Stand ina 28, hivyo mojawapo ikifungwa inaweza kuwa katika hatari ya kushuka daraja, hapo kazi itakuwepo.

Mjini Kagera kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, wenyeji Kagera Sugar wataivaa Prisons ya Mbeya ambayo ina pointi 28. Kagera wala haina madhara na matokeo yoyote yale lakini inaweza kukomaa na kuibania Prisons ambayo pia ipo katika hatari ya kushuka kama ikipoteza mechi hiyo.

Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Ndanda itaikaribisha Yanga kwenye mchezo unaoweza kuamua hatma ya timu hiyo pekee kutoka mikoa ya kusini katika ligi kuu ibaki au ishuke.

Inaweza kuwa mechi ya kisasi kwani Yanga ilibaniwa na Ndanda kwenye Uwanja wa Taifa na kutoka suluhu, hivyo licha ya kutwaa ubingwa inaweza ikaifunga timu hiyo yenye pointi 28 ili tu kuikomoa na kuishusha daraja.

Mechi nyingine itakuwa kwenye Uwanja wa Azam Complex ambapo Azam itacheza na Mgambo. Azam wala haina tatizo na matokeo yoyote yale, isipokuwa Mgambo iliyo nafasi ya 12 na pointi 28 na tofauti ya mabao ya hasi 10 inahitaji ushindi tu ili ibaki katika ligi.

Kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, timu ya Mbeya City yenyewe itakuwa haina cha kupoteza itakapovaana na Polisi Moro ambayo itahitaji ushindi mkubwa na kuziombea mabaya timu nyingine za chini ili ifufue matumaini ya kubaki ligi kuu. 

MECHI KALI ZA LEO JUMAMOSI 
Stand v Ruvu Shooting Kambarage, Shinyanga
Mbeya City v Polisi Moro Sokoine, Mbeya
Kagera Sugar v Prisons CCM Kirumba, Mwanza
Ndanda v Yanga Nangwanda, Mtwara
Azam v Mgambo Azam Complex, Chamazi Dar

MSIMAMO
TANZANIA BARA
                            P    W   D    L     GF  GA Pts

1. Yanga            25  17  4     4     52  17  55
2. Azam             25  13  9     3     36  18  48
3. Simba            25  12  8     5     36  18  44
4. Mtibwa         25  7     10  8     24  24  31
5. Mbeya          25  7     10  8     21  22  31
6. Kagera          25  8     7     10  22  26  31
7. JKT               25  8     7     10  19  23  31
8. Coastal         25  7     10  8     19  24  31
9. Ruvu              25  7     8     10  16  28  29
10. Prisons       25  5     11  7     18  22  28
11. Ndanda      25  7     7     11  20  30  28
12. Mgambo    25  8     4     13  18  28  28
13. Stand          25  7     7     11  22  34  28
14. Polisi           25  5     10  10  16  26  25

ZILIZO KATIKA HATARI
P    W   D    L     GF  GA GD Pts
9. Ruvu              25  7     8     10  16  28  -12 29
10. Prisons       25  5     11  7     18  22  -4   28
11. Ndanda      25  7     7     11  20  30  -10 28
12. Mgambo    25  8     4     13  18  28  -10 28
13. Stand          25  7     7     11  22  34  -12 28
14. Polisi           25  5     10  10  16  26  -10 25
NB: Ndanda na Mgambo zimefanana kwa tofauti ya mabao lakini Ndanda ipo juu kwa sababu ina mabao mengi ya kufunga.
© Copyright BURUDANIKA BLOG
Back To Top