Welcome

    Featured Posts

    BURUDANIKA BLOG - KWA MICHEZO NA BURUDANI ZOTE

    .

Loading...

HADITHI: DODO LIMEDONDOKA KWENYE MPERA …!

Hizi ni story za kufikirika, tafadhari, kama inaendana na eneo lolote halisi, picha au jina la mtu, ni kwa lengo la kuonesha uhalisia na kukupa uzoefu wa Ndani ya Bongo (Bongo Central). Waweza kutuma kwa E-Mail Story kama hizi za mjinikwenye e-mail: info@bongocentraltz.com


Jiji la Dar es Salaam ni jiji ambalo limesheheni mambo ya kila aina. Kuna ujanja, ujinga, wizi, utapeli, ujambazi, uasherati, umalaya, uchangudoa, ndoa za mkeka, fumanizi za kutengeneza, kuna biashara za kila aina.

Hapo kidogo umeniona kama narudia maneno yenye maana moja katika sentensi moja kama uasherati, umalaya na uchangudoa, lakini kila neon lina maana yake. Leo hatuelezani maana ya maneno bali ninataka tuzame uswailini kwetu.

Haya tu ni baadhi ya mambo yanayowatatiza wageni wa jiji hili wanapokuwa ndani ya Bongo (Bongo Central), kuna wageni wanaingia kila siku ndani ya muji huu uliojaa mambo mengi yaliyotajwa hapo juu japo mengine yamesahaulika. Fuatilia mkasa huu wa maisha nadhani utajifunza kitu, na kama una story kama hizi za kimjini zaidi, tupia kwa e-mail yetu: info@bongocentraltz.com . Pamoja tufundishane maujanja ya mjini…
________________________________________________


Kijana Davy alikuwa ni mtanashati na mtu wa kujituma sana darasani kwani alipokuwa chuo kikuu alikuwa anapata alama za kuridhisha. Mungu alimpa kipaji cha pekee cha uelewa wa darasani.
Katika kozi yake ya shahada ya kwanza ya Uongozi katika biashara katika chuo kikuu SAUT hapo Mwanza, Davy alipata wastani mzuri ambao hata wazazi wake walifurahi sana. Kitu cha pekee kilichokuwa kinamsumbua Davy ni jinsi ya kuyaanza maisha!

Nyumbani kwao Davy ni watu wenye uwezo ambao hawasumbuki pesa ya kununua mboga au unga. Katika mtaa wa Lumala C wilaya ya Ilemela jijini Mwanza, baba Davy anafahamika kuwa na malezi bora kwa watoto wake na anajitahidi kuwapeleka shule ili kuwawezesha kupata elimu itakayowasaidia hapo mbeleni.

Davy alipohitimu masomo yake ya chuo kikuu, aliwaomba wazazi wake wamsaidie mtaji ili aje Dar es salaam kuanza maisha na ajitenge na wazazi wake ili na yeye aanze kufanikisha baadhi ya ndoto zake katika maisha.

Wazazi walimuona Davy kakomaa kifikra na hawakujali, wakamsaidia kiasi Fulani cha pesa kwa ajili ya kupanga chumba cha kulala yaani ‘Geto’ na nyingine kwa ajili ya kula na kufanyia maombi ya kazi pamoja kununua vocha kwa ajili ya mawasiliano na hata kuweka ‘bando’ la ‘intaneti’ ili awe anaona matangazo mbali mbali ya kazi!

Ndoto za Davy zilikuwa nyingi sana. Miongoni mwa ndoto zake ni:-

1.     Kuwa na mke mrembo wa kuvutia nafsi yake.
2.     Kuwa nakazi ya maana ambayo inampa kipato kikubwa.
3.     Kumilki gari zuri kama GX V8, Harrier, Nissan Xtrail na mengine kibao.
4.     Kuwa na mjengo wa kuleta heshima.
5.     Kumilki kampuni kubwa sana amablo litafahamika Tanzania na Afrika mashariki yote!

Si malengo hayo tu ila ni malengo ambayo yanalenga maisha bora tu! Davy ndo zilikuwa ndoto zake kuwa kiongozi katika taasisi kubwa ya kipesa lakini ….!

Davy hajawahi kuwa na mpenzi wa kudumu kabisa bali alikuwa anapata wapenzi wa kisiri siri kwani malezi ya familia yake yalikuwa ni ya ‘geti kali’. Kwa kuwa ameshapewa pesa ya kuishi Dar es salaam (Bongo Central), aliona ndo fursa pekee sasa ya yeye kutumia muda wake kutafuta wapenzi kwani alikuwa anatamani sana kuwa na mpenzi mrembo sana mwenye ‘mauzo’ ya kila aina!
**************************************
Baada ya miezi tisa akiwa ndani ya jiji la Dar es salaam, Davy alianza kuona mambo yanakuwa magumu tu tofauti na jinsi alivyokuwa akidhani kuwa ni mteremko tu! Alipata vijikazi vidogo vidogo katika makampuni tofauti tofauti na alikuwa akijipanga kimaisha zaidi.
Kitu kilichokuwa kikimsumbua ni kupata mrembo tu! Ni hali iliyokuwa inamfanya usiku asilale akikesha anaangalia filamu za Kibongo akiangalia warembo tu ili aone mtu atakayemchagua atafanana na huyo ‘Star’ wa kwenye filamu anayoangalia.

Siku moja Davy akachelewa kurudi nyumbani isivyokawaida yake. Alirudi kwenye muda wa saa moja na nusu ambapo kawaida huwa anarudi saa kumi jioni na anaanza kazi yake ya kuangalia warembo kwenye filamu mbali mbali. Basi, akapitia njia ile ile anayopita mara kwa mara. Kabla ya kumaliza mtaa mmoja ili afike kwake, huwa kuna njia ambayo ina mambo mengi ya starehe za kimjini kama vile Baa, miziki sana tu ambapo warembo akawakuta wapo njiani anapopitia yeye. Ghafla akashikwa mkono huku akiambiwa, ‘Halo mpenzi, ni shilingi elfu mbili tu unanichukua, gharama za chumba ni elfu moja, jumla ni elfu tatu tu fasta…’. Huku akishikwa maeneo yasiyo na adabu, Davy akajikuta anaropoka, ‘Si twende kwangu…’.

Binti Yule alikuwa ni mrembo kupitiliza. Ni miongoni mwa warembo ambao Davy huwa anawawaza kuwaoa. Binti akamwambia Davy kuwa atoe shilingi elfu ishirini kama anataka ampeleke getoni kwake wakakae mpaka asubuhi. Davy hakusita, kwani nyumbani alikuwa na shilingi elfu hamsini, na mfukoni alikuwa na shilingi elfu kumi na saba na mia mbili!

“Twende tu usijali”, Davy alimwambia binti. Binti akawaaga wenzake na kuelekea kitaa cha akina Davy. Walipofika ikabidi wakatafute chakula kwanza kwani Davy kwake hakuna dalili yoyote ya msosi kama msela, alimpitisha kwa jirani zake huyo mrembo ili wajue kuwa Davy ni kidume…
Binti alipofika ndani akajitambulisha kwa jina la uongo ambapo alijiita Tatu kumbe anaitwa Mwanne! Davy yeye hakuchelewa kujitambulisha kiukweli, “ Naitwa Davy, ni mhitimu wa chuo kikuu na ninafanya kazi Bongo Sound Media Company limited, ni kampuni ambalo lipo posta na ninafanya kama part time kwani sijaajiriwa kabisa, kwetu ni Mwanza, ni msukuma”.

Kama kawaida, Dodo limedondoka kwenye Mpera! Davy alimpenda sana binti huyo kwa muda mfupi tu walioonana! Davy wetu akaenda kuoga na kumwamini kabisa huyu changu aliyemzoa njiani. Binti alipobaki peke yake akaanza kuyaandaa mazingira ya mambo ya jiji sasa! Kwa kuwa davy wetu bado hajakutana na miamba kama hii, yeye aliona kapata kumbe kapatikana na hapo ndo aanze upya na kwa aibu kubwa sana.

Alipotoka bafuni akamkuta binti kajiachia kama alivyozaliwa na amejilaza kitandani kasha akamuomba Davy wetu amuwekee filamu nzuri ya Kibongo aangalie akimwambia maneno machache tu, “ baby, mbuzi kafia kwa muuza supu”. Davy akadakia akisema kama mbuzi kafia kwa muuza supu si ndo bahati kwa muuza supu kujipatia nyama fasta tena ya bure. Davy hakuielewa misemo hii na aliielewa baada kuwa limetokea la kumtokea.

Wakaangalia filamu mpaka saa tano usiku ndipo Davy akaanza kusikia ka “usingizi” ndipo alipojilaza. Binti alikuwa ameyaweka sawa mazingira ya kazi! Alikuwa ana makucha marefu ya kimahaba kumbe yamejaa “unga a.k.a Sembe au madawa ya kulevya”. Walipokuwa wanaangalia filamu nzuri ya Kibongo, Tatu feki alikuwa akimtomasa tomasa Davy wetu ambaye alionekana kama “Mbugila” Fulani hivi …

Wakati anashikwa shikwa mwili mzima, makucha ya Tatu feki yalikuwa hayachelewi kufika puani kwa Davy! Kumbe unga ndo ulikuwa unasogezwa puani kwake pasipo kujua… maskini Davy!
Basi usingizi ulipokolea, binti akabofya simu ya mkononi kuwasitua masela wake aliowaaga kuwa anaenda ku-kazi! Akawaandikia meseji kuwa tayari “Mbuzi kafia kwa muuza supu, waje wachukue nyama tu”.

Kama kawaida ikachukuliwa gari ndogo ya mizigo ikaja mpaka hapo kwa Davy wakati wapangaji wengine wapo ndani. Wlichukua kila kitu mpaka zulia, nguo na hata vyeti vyake vyake. Wakachukua ufunguo wa kitasa cha mlango wakaufunga mlango vizuri kasha wakaidumbukiza ndani funguo hiyo…

Tatu feki katokomea kusikojulikanika, Davy wetu anaamka asubuhi anakuta majanga tupu. Kwanza akalala tena maana alifikiri yupo ndotoni! “Mbuzi kafia kwa muuza supu… Tatu kaniibia jamani…. Au nipo kwa jirani nimekosea njia!... au nipo wapi maana hata picha za ukutani sizioni…”
Akaamka alipojikagua vizuri akakuta hata “Duka” limevunjwa maana alianza kusikia maumivu makali sana. Ndo akaamua kufungua mlango akiwaomba jirani zake wamsaidie kwenda polisi na kumpeleka hospitali.

 **************************************

Ilikuwa ni aibu kwa Davy kuwasimulia nyumbani kwao kwani ni aibu sana. Akawapigia simu na akawadanganya kuwa amevamiwa na majambazi nyumbani kwake na wamechukua kila kitu akabaki na kipensi tu tena kidogo dogo ambacho hawezi kukivaa hadharani ila jirani zake wamemsaidia nguo baadhi za kumsaidia.

Polisi walipokuja wakaanza kuangalia mazingira jinsi alivyovamiwa wala haileweki maana hana vitu vya kumfanya jambazi aache kulala aje amuibie yeye sijui godoro na kitanda vitu ambavyo havileti maana yoyote. Na hakuna dalili yoyote ya jirani kufahamu wizi huo bali yeye tu. Walipowahoji vizuri jirani zake wakatililika kama kawaida yetu mjini umbea ndo kazi yetu, yakaelezwa yote kuwa alifikiri kapata mchumba kumbe “Dodo limedondoka kwenye mpera”.

Ilikuwa ni aibu kwa wazazi wake Davy na hata yeye mwenyewe! Alikuwa akisikia unga tu anadhani unga ni wa mateja tu…..
© Copyright BURUDANIKA BLOG
Back To Top